|  | 
| Kikosi cha timu ya taifa ya Brazil alamaarufu Samba Boys | 
   Brazil na Colombia zitamenyana kwenye mchezo wa 
robo fainali ya  Kombe la Dunia hii leo mchuano huo utakaragaziwa  Uwanjani Castelao mjini 
Fortaleza.Mara ya mwisho Colombia kuilaza  Brazil ilikuwa 
mwaka 1991. Lakini, kipute hicho cha robo fainali ya Kombe la Dunia 
kinaikuta Colombia ikiwa kwenye ubora mkubwa na kuundwa na nyota makini 
akiwemo Rodriguez, Juan Cuadrado na Jackson Martinez na kuwafanya Brazil
 kuwa kwenye presha kubwa sana.Cuadrado, ndiye mchezaji aliyepiga pasi nyingi 
zilizozaa mabao kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia, akiwa amechangia 
mabao manne kwa kikosi cha Colombia.Kwenye hatua ya 16 bora, Brazil ilipata shida 
dhidi ya Chile na kufanikiwa kuwatupa nje kwa mikwaju ya penalti 3-2, 
wakati Colombia iliichapa Uruguay kiulaini mabao 2-0, shukrani kwa mabao
 hatari ya Rodriguez na kazi nzuri ya staa wa taifa hilo, Cuadrado.Utamu wa mchezo huo utazikutanisha timu mbili 
zinazobebwa na mastaa vijana, Neymar kwa upande wa Brazil na Rodriguez 
kwa Colombia. Kwenye fainali hizo, Neymar ametikisa nyavu mara mbili, 
moja pungufu ya mpinzani wake wa leo, James Rodriguez. 
 
|  | 
| Radamel Falcao Strika wa Colombia | 
Robo fainali hiyo itatanguliwa na ile kati ya 
Ufaransa na Ujerumani itakayopigwa kwenye Uwanja wa Maracana jijini Rio 
de Janeiro. Mechi hiyo ya Ufaransa na Ujerumani ni ya kihistoria.
 
Timu hizo mbili ziliwahi kumenyana kwenye hatua ya
 nusu fainali ya Kombe la Dunia 1982, ambapo Wajerumani walishinda kwa 
mikwaju ya penalti. Ufaransa itaingia kwenye mchezo huo ikitaka kulipa 
kisasi, lakini jambo hilo litafanywa na wachezaji 21 kati ya 23 kwenye 
kikosi hicho cha Les Bleus ambao walikuwa hawajazaliwa wakati timu yao 
ikifungwa kwa penalti na Ujerumani katika fainali hizo.Kiungo Blaise Matuidi atabeba majukumu ya Ufaransa
 kwenye sehemu ya kiungo sambamba na Paul Pogba na Yohan Cabaye, ambao 
watakuwa kwenye vita ya nguvu dhidi ya Toni Kroos, ambaye amefunika kwa 
kupiga pasi katika fainali hizo za Brazil.Aidha mechi nyingine za hatua ya robo fainali 
zitaendelea kesho,ambapo Argentina itakajimwaya uwanjani  na Ubelgiji 
na Uholanzi itakapokwaruzana na Costa Rica.
Said PiePie,Nairobi