Rais wa Brazil Dilma Rousseff
amewaomba wananchi nchini humo kuungana
pamoja kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2014, akisema taifa liko tayari licha ya Migomo
na maandamano ambayo yameshuhudiwa nchini humo.Katika hotuba yake iliyorushwa
kwenye televisheni kabla ya ufunguzi wa tamasha hilo, rais huyo amesema macho
ya ulimwengu mzima yanaiangazia Brazil akisema nchi hiyo ilikabiliana na
changamoto kubwa na sasa iko tayari ndani na nje ya viwanja kwa ajili ya
burudani hilo la soka.
Huku hayo yakijiri vitisho
vilivyokuwepo vya mgomo vimeondolewa kwa
muda huku wafanyakazi wa treni za chini ya ardhi mjini Rio wakiufutilia mbali
mgomo wao baada ya kupewa nyongeza ya mshahara ya asilimia 8. Mgomo wa siku
tano wa usafiri mjini Sao Paulo pia ulisitishwa Jumatatu wiki hii, ijapokuwa
huenda ukarejea tena wakati michuano itakapoanza kama wafanyakazi waliopigwa
kalamu hawatorudishwa kazini.
Sherehe za ufunguzi wa dimba hilo
zinaandaliwa katika uwanja wa Corinthians Arena, mjini Sao Paulo hii leo, miongoni
mwa wageni watakaohudhuria ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
pamoja na viongozi 12 wa nchi na serikali.
Baada ya sherehe za ufunguzi, vijana
wa kocha Luiz Felipe Scolari, watashuka dimbani kupambana na Croatia katika
mechi ya ufunguzi ya Kundi A. Na kama wenyeji hao wataweza kufika katika
fainali na kunyakua taji hilo mnamo Julai 13, watakuwa timu ya tatu pekee
iliyocheza mechi ya ufunguzi kuwahi kufanya hivyo.
Katika michuano 19 ya Kombe
la Dunia, Italia pekee mwaka wa 1934 na England mwaka wa 1966
zilizowahi kucheza mechi ya kwanza na kushinda katika fainali. Zaidi ya
wanajeshi na polisi 150,000 watashika doria k wakati wa dimba hilo.
Said PiePie,Nairobi