Wednesday, 9 July 2014

BRAZIL WAANGAMIZWA NA WAJERUMANI



     
David Luiz ashangaa baada ya kulazwa na Ujerumani
     Mchecheto wa timu ya Brazil kunyakua Kombe la Dunia mwaka huu ulizimwa hapo jana baada ya Ujerumani kuwarindima  mabao 7-1 katika uwanja wa Estadio Mineirao ulioko Belo Horizonte.
 Hicho ndicho kilikuwa kichapo kikubwa kuwahi kutokea  katika historia yao ya miaka 100 ya soka.
Kocha Luiz Felipe Scolari aliyeonekana kupatwa na mshangao mkubwa,amewaomba mashabiki wamsamehe  kutokana na makosa waliyofanya. Rais Dilma Roussef pia alituma ujumbe wa kuituliza mioyo ya mashabiki.Thomas Müller ambaye alifunga goli lake la tano katika dimba hili, alisema hawakuamini matokeo hayo ya kushangaza. Tikiti ya Ujerumani kuelekea mjini Rio ilipatikana baada ya kipindi cha kwanza cha maangamizi ambacho walifunga magoli manne katika dakika sita.
 Thomas Müller alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 11 kutokana na mkwaju wa kona. Miroslav Klose kisha akatia kimyani la pili katika dakika ya 23 ambalo lilikuwa lake la 16 na kumfanya kuwa mfungaji wa magoli mengi katika historia ya Kombe la Dunia.


Kilio cha mashabiki wa timu ya Brazil hakikuzulika
Mashabiki wa Brazil hawakuamini macho yao namna timu yao ilivyokalifishwa uwanjani kutoka mwanzo.Toni Kroos alifunga  katika dakika ya 24 na 26 mtawalia ili kufanya mambo kuwa 4-0 na kisha Sami Khedira akabusu wavu na kufikisha 5-0 katika dakika ya 29.Goli la dakika ya mwisho lake Oscar la kufutia machozi hata halikuwatikisa mashabiki wa Brazil ndani ya uwanja. Kocha wa Ujerumani Joachim Löw amesema Brazil walishtuka baada ya kufunwga magoli ya mapema, kwa sababu hawakutarajia hilo. Hawakujua wafanye nini. Safu yao ya ulinzi haikuwa imejipanga. Ujerumani sasa wanajiandaa kwa fainali itakayochezwa katika uwanja wa Maracana Jumapili tarehe 13. Na mpinzani wao atajulikana hiii leo, kati ya Argentina na Uholanzi ambao wanakutana katika nusu fainali ya pili.



Said PiePie,Nairobi.